Tuesday, August 12th, 2008

Barabara ya msimu Makete!

Hari ya barabara wilayani Makete wakati wa masika.picha kwa hisani ya Habari leo.

Hari ya barabara wilayani Makete wakati wa masika.picha kwa hisani ya Habari leo.

Napenda kuchukua nafasi hii tena kuwakaribisha katika mazungumzo yetu ya leo katika kona ya barua ya kila wiki toka kwangu rafiki na ndugu yenu Nidekile.

 

 

 

 

Kwa walioko Makete pole na heka heka za kumpokea mheshimiwa Rais nasikia alikuwa Iwawa. Nasikia viwanja vya mabehwani mahali ambapo Mh. Rais alihutubia palikuwa hapatoshi maana watu walifurika toka kila kona, sijui kama ndugu zetu wa Kigulu walikuwepo?. Huu ndio wakati hasa huwa tunawakumbuka. Kwani wakija na ngoma yao ya Ling’oma basi huwa ni burudani  tosha kutugandisha macho wakinga wa milimani.

 

Mwenge au ugeni ukishapita basi tunasahau kabisa habari za kata ya Kiguru. Kiguru ni kata inayotupa matunda mbali mbali ambayo hayawezi kusitawi katika hali ya baridi kali na miinuko kama ya ukanda wa juu Makete.

 

Matunda kama ndizi, maparachichi, machungwa na mengine unayoweza kuyataja hutoka katika kata hii. Kata hii inatoa pia mazao kama kahawa na chai na viungo kama pilipili, binzari na tangawizi ambazo wakazi wa Makete milimani huzitumia.

 

Lakini vitu hivi huozea shambani, havifiki katika masoko yanayoizunguka Kigulu, Makete na Tukuyu. Wakati mwingine huwa yanavunwa na huozea katika maghara ya wakulima.

 

Kigulu sio kata pekee inayopata tatizo la usafiri. Akiwa wilayani Makete Mh. Rais alimwomba Mwenyekiti wa kijiji cha Iwawa kutoa kero kwa niaba ya wananchi. Mwenyekiti alilamika na kuongea kwa uchungu juu ya tatizo la barabara wilayani Makete.

 

Katika kujibu kero hiyo Rais alimwagiza Mhandisi wa mkoa ambaye naye alikuwepo katika mkutano huo kuhakikisha sehemu korofi zote zimerekebishwa. Hata hivyo Rais aliongeza kuwa serikali imetenga jumla ya shilingi. Milioni mia nne kwa ajili ya ujenzi wa barabara  hiyo.

 

Sio mara ya kwanza kusikia malalamiko ya wananchi wa Makete juu ya ubovu wa barabara wilayani kwao. Na wala sio ajabu kusikia kuwa kiongozi wa juu ametoa oda ya kuwa barabara ya Makete itengenezwe mara moja. Lakini miaka imekuwa ikipita na hatuoni mabadiliko yoyote. Kulikoni?

 

Akishangiliwa na wananchi Rais alisema barabara hii mwaka huu ni lazima itengenezwe na sehemu korofi ziwekewe lami ikiwa ni hatua za mwanzo za kuelekea kujenga barabara hii kwa lami. Na ujenzi wake uanzie Makete kuelekea Njombe.

 

Barabara Makete imekuwa ni kwakwazo kikubwa kwa maendeleo na usatawi wa jamii ya wana Makete. Mwaka juzi kufuatia ubovu wa barabara Mkuu wa wilaya ya Makete alilazimika kufunga barabara ya Njombe Makete na kuhakikisha haitumiki kwa mwezi mzima na hata alipotangaza kuifungua ilikuwa haiwezekani kupitika tena.

 

Mwaka jana nao kwa miezi mitatu mfulurizo  barabara ya Makete haipitiki. Watu tuliacha kwenda Makete, tulitenganishwa na familia zetu ambazo zinaishi huko. Shida ni nini hasa?

 

Uongozi wa Halimashauri ya wilaya ya Makete haoneshi kama unaona barabara ni tatizo. Haujaiweka barabara katika ajenda zake za kudumu. Wanasiasa wanapoongea katika mikutano ya siasa wana kwepa kwa makusudi kabisa kugusia suala la barabara kwa kujitetea kuwa barabara ya Makete ni barabara ya Taifa kwa hiyo mwenye jukumu ni TANROAD

 

Ukiwauliza wao sasa barabara zao walizoshughurikia ni zipi? mbona hatuzioni? Ziko wapi barabara ambazo madiwani na watendaji wao wa kata wanazisimamia? Iko wapi barabara ambayo mkurugenzi na Afisa mipango wameipa kipaumbele?

 

Ipo wapi barabara ambayo mwenyekiti wa Halimashauri na mheshimiwa mbunge wanaweza wakasimama mbele za watu wakasema sisi ndio viongozi wenu, na tumefanikisha kuwezekana usafiri kwa wanamakete nje na ndani ya wilaya kupitia barabara hii.

 

Wanasiasa wetu wamepoteza muda wa miaka yote mitatu toka tumewachagua kwa kulumbana. Wamelumbana kwa masuala yasiyo na tija, wametafutiana fitina kwa nia ya kulinda nafasi zao, kwa maslahi yao binafsi, si kwa nia ya kuwasaidia wananchi wa Makete. Wamesahau kuwatumikia wale waliowapa kura, wamewasahau kabisa wananchi na ahadi zao walizowaahidi za kwenda kwa kasi kubwa kuliko ya mwanga wa jua.

 

Makete inahitaji msukumo mpya, Makete inahitaji kizazi chenye fikra mbadala. Viongozi walio bora na walio na dira , wanaojua wapi wanataka kuwapeleka wananchi wao. Hatuwezi kuwa na matumaini na maisha bora kama viongozi wetu ndio hawa, tunaonana nao akija Rais. Wote wanamakazi yao mijini.

 

Hatuna sababu kuwa masikini na wilaya kama hii yenye kila aina ya utajiri. Maendeleo yaliyopo sasa Makete ni juhudi za wanamakete za Miaka ya sitini. Hakujawa na juhudi mpya tena. Nyumba za tofali za kuchomwa na kuezekwa kwa bati, dispensary, hospitali nzuri zote zimejengwa miaka hiyo!

 

Tunahitaji mabadiliko. Na mabadiliko ya kweli ya kiuchumi yataletwa kwa kuweka miundombinu kama barabara nzuri inayopitika mwaka mzima.

 

Ngoja nikamalizie kuanika vitofali vyangu kabla kamvua hakajaja, maana nisipomaliza kujenga kabla mvua haijaanza ikinikuta sitaweza kusafirisha mabati mapaka eneo la ujenzi. Barabara bila shaka itakuwa haipitiki tu, anyway yetu macho ngoja tusubiri tuone?

 

 

 

 

Jackson Mbogela

Nidekile                                                                                       

 

2 Responses to “Barabara ya msimu Makete!”


  1. Royal Orr says:

    Great to see new material on the site. Keep it up PIUMA! Congratulations to Jackson and the communications team of Juma and Witness for this.


  2. malila says:

    Hali ya nyumbani Makete inasikitisha sana,barabara zote ni mbovu kuanzia zile za tanroad na za H/shauri.

    Jamani malumbano ya viongozi wetu ni hasara kwetu. Wanamakete viongozi wetu wote tukianzia na madiwani wetu Makete ndio kwetu hivyo ni wajibu wetu kuijenga makete.

    Na ninyi mnaolumbana jueni kuwa mnatuchelewesha,Makete iko nyuma.

Leave a Reply