Wednesday, October 8th, 2008

Nadharia ya Haki ya Matibabu

Wiki hii ukurasa  wa PIUMA umebeba habari ya msichana Veneranda Sanga. Msichana ambaye yupo kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Bulongwa wilayani Makete.

Kama walivyo watoto wengi wilayani Makete, Veneranda ni mtoto yatima aliyepotelewa na wazazi wake katika umri mdogo sana katika kijiji cha jirani cha Iniho. Nilikutana na Veneranda wakati nafanya kazi na PIUMA na kusaidia kituo cha tiba ya UKIMWI cha hospitali ya ya misheni ya Bulongwa mwezi wa sita 2005.

Nilipoonana na Veneranda alikuwa tayari kwenye maangalizi katika kituo cha Tiba ya kupunguza makali ya Ukimwi katika hospitali hiyo, kilichokuwa kikiendeshwa na madaktari wakujitolea wa kutoka shirika la kidini la EAWM huko Austria.

Wakati Fulani madkatari wasio na Mipaka MSF-Spain walifika Bulongwa kwa ajili ya kutoa mkono wa msaada kwa kituo hicho ambacho kilikuwa tayari na wagonjwa 600 wanaohudumiwa na Daktari mmoja , nesi  na mtu wa maabara mmoja.

Hali ya Afya ya Veneranda haikuwa nzuri ingawa alikuwa kwenye dawa kwa kipindi cha miezi sita. Alikuwa na homa za hapa na pale na alikuwa akitokwa na majipu hasa kichwani. “Hatutegemei mabadiriko ya haraka na ghafla kwa mgonjwa anayeanza kutumia dawa za ARV ila kadri muda unavyoenda na jinsi atakavyokuwa anafuata ushauri na kutumia dawa vizuri, ndivyo atakavyozidi kuboreka” nakumbuka yalikuwa majibu ya Daktari wa Veneranda, Dokta Rainer Brandl nilipomuuliza kama niwe na matumaini na Veneranda hata kama afya yake ina suasua.

Kwa vile dakatari huyo alitaka kuhakikisha kuwa Veneranda anapata tiba ya uhakika alimuombea makazi katika kituo cha yatima ambapo alipata nafasi ya kuishi, na kumweka chini ya uangalizi wa karibu wa nesi  Mary Musoma wa PIUMA na Betty Liduke wa TANWAT.

Afya ya Veneranda ilizidi kuimarika chini ya msaada Manesi  hawa ambao walifuatilia kwa karibu afya ya binti huyu ambaye wakati huo alikuwa Darasa la tano. Nilipomwona mwaka 2007 wakati anaanza kidato caha kwanza  sikuamini kama ni yule yule Veneranda niliyemwona miaka miwili iliyopita. Kwani sasa alikuwa ni mrembo na mwenye afya nzuri, uso uliojaa tabasamu na sura ya kuvutia.

Veneranda alipata nafasi ya kusoma sekondari baada ya wafadhiri wa nje kujitokeza kulipia gharama za masomo yake. Hata hivyo Veneranda hakuwa mwenye matumaini na ujasiri kama alivyokuwa huko nyuma.

Matumaini na Ujasiri wa Veneranda vilitoweka kwani Madaktari waliokuwa wakimtibu walikuwa wamefukuzwa na kanisa wamiliki wa hospitali kwa kushindwa kukabidhi pesa zilizotolewa na wafadhiri wa nje kwa ajili ya kuendeshea kituo kwenye mikono ya viongozi wa kanisa. Pia kwa kukemea kwao wazi wazi wizi uliokuwa ukiendelea katika hospitali ya Bulongwa. Wizi wa Pesa za kuendeshea hospitali zikiwemo pesa za UKIMWI.

Kuondoka kwa madaktari hao, kulimkosesha Veneranda msaada wa manesi wa karibu na hata ufuatiliaji ulipungua. Kwani hakukuwa na utaratibu kulipia gharama hizo tena.

Leo Veneranda amelazwa hospitali akiwa kwenye mdripu, amekuwa ni mgonjwa kitandani kwa miezi kadhaa sasa, na afya yake inaripotiwa kuwa imekuwa ikizorota kila siku. Hali ya kula sio nzuri, hana mtu wa kumtunza zaidi ya wanafunzi na watoto wenzie wanao ishi naye katika kituo cha yatima. Ambao hawawezi kuwa karibu naye wakati wote kwani wanahitaji kwenda shule na kujisomea.

Nilipozungumza na Juma Nzige Daktari wa PIUMA ambaye alifika kuona afya ya Veneranda, alisema madaktari wa hospitali anayotibiwa Veneranda wanawasiwasi kuwa Veneranda hajatumia vizuri dawa zake za kupunguza makali ya UKIMWI, ingawa Veneranda mwenyewe anasema amekuwa akitumia dawa zake bila kukosa kila siku.

Kutokana na hilo Juma anahisi kuwa Virusi vya UKIMWI Mwilini mwa Veneranda vinawezekana vimejenga Usugu (resistance), na Veneranda anahitaji vipimo zaidi kujua kama hili tatizo lipo au la. Na kama Virusi mwilini mwa veneranda vimejenga usugu  Veneranda atahitaji kubadilishiwa dawa, kutoka First line regiment kwenda kwenye dawa ambazo wanaziita second line regiment.

Kwa kufanya hivyo tunaweza tukaokoa uhai wa mtoto Veneranda tena. Naamini matibabu bora ni haki ya kila mtu. Ingawa sijasikia kama Makete ambako waathirika ni wengi dawa hizi zimeaanza kutolewa, lakini nimeshaoona wanaharakati wengi wanaoishi na virusi vya UKIMWI hapa nchini wakitumia Dawa hizi.

Wakati akiwa na afya Veneranda aliwashawishi watoto wenzake wengi  kupima, na pia alikuwa ni msaada wa ushauri kwa watoto wanaoishi na virusi vya UKIMWI hasa ambao walikuwa waanze kutumia dawa. Ametokea mara kadhaa katika magazeti na redio. Amehusika katika uhamasishaji na kutoa semina kwa WaVU. Hakuletwa na mtu kwenye kituo cha kupimia, alienda pekee yake kwa kutembea kwa miguu umbali wa kilomita saba.

Kituo cha Yatima Bulongwa kinajumla ya watoto wasiopungua wanne wanaoishi na Virusi vya UKIMWI wote wakiwa chini ya miaka 12. Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii ionyeshe kuwa tiba ni haki ya kila mtu, imwangalie Veneranda Makete, yeye hahitaji kupelekwa India wala Afrika Kusini. Anachohitaji Veneranda Damu yake ichunguzwe kama vimelea vimeota usugu katika maabara zetu za hospiali za rufaa kama Mbeya (kilomita 90 toka Bulongwa)  alafu apewe dawa zitakazo endana na ugonjwa wake.

Upone haraka Ven

Nidekile!

Leave a Reply