Ufugaji wa Samaki.
Na Evance Seth.
Katika hali ya kawaida kwa mtu ambaye amefika Wilayani Makete hawezi kutegemea kusikia habari ya samaki wabichi pamoja na ukweli kwamba wilaya hii kuwa na utajiri wa mito mingi, mikubwa na inayotiririka mwaka mzima lakini ni vigumu kuhisi kuwepo kwa samaki.
Upatikanaji wa samaki ni mgumu kwa sababu wilaya hii ina milima mingi hivyo maji yake kutiririka kwa kasi kubwa kuelekea ziwa nyasa au bonde la usangu.
Kutokana na kujua umuhimu wa zao la samaki wananchi wa Wilaya ya Makete wameanzisha kilimo cha ufugaji wa samaki kwa njia ya Mabwawa. Akizungumza na mwandishi wa habari hii Bwana Ilomo mmoja wa wafugaji wa samaki hao alisema kuwa yeye alianza mradi wa ufugaji wa samaki mwaka 2005.
Alipokuwa akichimba hilo bwawa watu walimcheka sana kufuatana na sehemu yenyewe jinsi ilivyokuwa na ugumu, kwani palikuwa na chemichemi. Pamoja na kuwa hakuwa na mbegu ya samaki lakini aliendelea kuchimba hayo mabwawa mpaka yalipofika matano.
“Kwa bahati nzuri binti yangu alinitafutia mtaalamu wa samaki Bwana Lingambe toka kijiji cha Utanziwa ambaye alikuja kuangalia jinsi mabwawa yalivyochimbwa” alisema Bw. Ilomo. Mtaalam wa samaki Bw. Lingambe alipoona mabwawa hayo yanafaa kwa ufugaji wa samaki alimuuzia Bw. Ilomo mbegu wa samaki aina ya Pelege mia tatu, wakati huo mbegu mmoja wa samaki alikuwa anauzwa kwa shilingi mia moja.
Aliendelea kusema kuwa ulipotolewa mkopo kwa wajasiliamali kutoka kwa Mh. Jakaya Kikwete, alitaka kuongeza mtaji kwa kwenda kukopa mkopo huo, lakini kutokana na masharti kuwa magumu alishindwa kupata mkopo huo.
Bw. Ilomo ansema alihitaji mtaji zaidi kwa ajili ya kuongeza mbegu zingine, kununua mabomba pamoja na kuinua kingo za bwawa. “Nilihitaji kama shilingi milioni moja tu” aliongeza Bw. Ilomo huku akionyesha sura ya masikitiko. Lakini alipowasilisha maombi yake benki aliambiwa na watoa mikopo hiyo kuwa wanakopesha kuanzia shilingi laki tano tu, na hizo fedha zinatakiwa kulipwa ndani ya miezi sita, kwa hiyo alishindwa kupata fedha hizo.
Lakini hakukata tamaa alitafuta namna nyingine kuweza kupata pesa aliyoitumia kwa ajili ya kununulia vifaa vilivyokuwa vinahitajika kwenye mabwawa hayo. Kwa sasa ana samaki wengi, ambao huwa anavua kwa ajili ya kujipatia kitoweo pamoja na kuwauza, na samaki mmoja huwa anamuuza kwa bei ya sh. 500 – 1000.
Hata hivyo Bwana Ilomo alisema kuna matatizo mbalimbali ambayo huwa anayapata hasa maji yanapojaa sana samaki hutoka nje na kusababisha hasara kwake, ukosefu wa zana za uvuvi, kukosa elimu ya ufugaji na uvuvi, samaki kuliwa na ndege pamoja na fisimaji, mtaji bado haujitoshelezi na uhaba wa soko la samaki.
Pamoja na changamoto anazozipata alisema kuwa kwa sasa anatumia dawa ya Letside kuua ndege na fisimaji kwa kumpaka samaki aliyekufa na kumweka kando ya bwawa na ndege hao humla huyo samaki na huenda kufa.
Mwisho alisema kuwa lengo lake kuu ni kuongeza samaki wa aina zingine, kuelimisha jamii inayomzunguka juu ya ufugaji wa samaki, kwani tangu aanze kufuga hao samaki na kuuza amefanikiwa kujipatia fedha kwa ajili ya kujikwamua matatizo mbalimbali.
Katika tarafa za Magoma na Bulongwa wilayani humu wanachama wa PIUMA nao wamekuwa wakiendesha miradi ya ufugaji wa samaki kwa njia ya Mabwawa.
Mzee Ilomo akiwa kwenye mabwawa yake.


Jackson says:
Mzee Ilomo is the first person in this village to install a solar powered system in his house and had TV setellite dish. Such people if supported they can influence community for self reliance.
malila says:
Huyu mzee yupo kijiji gani ? Je nikitaka kufika kwake,nikiwa Makete napanda magari ya wapi? Nataka siku moja nikifika makete nikamwone huyo mzee.