Wednesday, June 10th, 2009

Mtikisiko wa uchumi wa Dunia kuokolewa na biashara ya Ulanzi!!

 

Na Evance Seth.

 

Pamoja na uchumi kuyumba kidunia wananchi wa Makete hawajakata tamaa  katika utafutaji wa maisha kwa kutafuta fedha kwa njia mbalimbali ambazo ni halali. Pombe ya kienyeji itokanayo na miti iitwayo mianzi imekuwa ni sehemu ya chanzo cha mapato kwa sehemu kubwa ya wanamakete.

 

Kutokana na ugumu wa maisha wananchi wengi wa Wilaya ya Makete wanajishughulisha na biashara ya ugemaji na uuzaji wa Ulanzi. Akizungumza na mwandishi wa habari hii Bwana Kenedy Kayamba  mkazi wa kijiji cha Maturunga mmoja wa wagemaji wa ulanzi alisema kuwa yeye alianza biashara hii mwaka 2004.

 

Alisema kuwa alipewa  urithi wa vitindi na babu yake “wakati babu bado yupo tulikuwa tunaenda wote kugema na kunifundisha jinsi ya kugema, alinifundisha jinsi ya kupanda alisema kuwa  niwe nachomeka kitindi mshazari, niwe nagema  mara mbili kwa siku asubuhi na jioni na kuosha mbeta kila baada ya siku mbili. Nilifuata masharti ya babu na hatimaye nikafanikiwa , mwanzoni nilikuwa nagema lita kumi kwa siku, siku zilivyokuwa zinazidi kwenda lita za ulanzi zikazidi kuongezeka na hatimaye kwa sasa nagema lita ishirini kwa siku” alisema Bw. Kayamba.

 

Aliendelea kusema kuwa biashara hii ni ya msimu kwani  inategemea mvua , wakati wa masika ulanzi huwa mwingi lakini biashara yake huwa sio nzuri kwani lita moja huuzwa kwa shilingi mia mbili na wakati wa kiangazi lita moja huuzwa kwa shilingi mia tano.

 

Alisema kuwa kwa kuwa biashara ni mbaya wakati wa masika, kwa hiyo wanachokifanya kwa sasa  ni kununua madumu mengi yenye mifuniko na kugema ulanzi  kuujaza  kwenye madumu hayo, baada ya hapo wanaenda kuyafukia kwenye chemichemi za maji au sehemu yanapopita maji kidogo kwa ajili ya kuuza kiangazi, Kwa hiyo wanapofukia madumu hayo chini ya ardhi ndio friji lao, kwani ulanzi unaweza kukaa kwa muda wa miezi zaidi ya mitano na ukawa bado mzuri.

 

Hata hivyo  Bwana Kayamba alisema kuna matatizo mbalimbali ambayo huwa anayapata ni pamoja na kung’atwa na nyuki akiwahi kwenda kugema kwani nao huwa wanakuwa wamelewa. “Mpaka sasa hivi hatuna soko la uhakika la mazao ya ulanzi hatuwezi kuuza kwa faida” aliongeza Bw. Kayamba

 

Lakini pamoja na changamoto hizo alisema kuwa mipango yake ya baadaye ni kuongeza shamba la vitindi, na kuidumisha biashara yake iwe ya kudumu kwa kiangazi na masika, kwa kuvitunza vizuri vitindi vyake kwa kuvipalilia ili aweze kugema ulanzi hata wakati wa kiangazi.

 

Marafiki wa PIUMA kutoka Kanada, Canadians Friends of Higlandshope walikuwa nafikiria kutafuta njia rahisi itakayoweza kuwasaidia wakulima wa ulanzi kutengeneza utomvu mzito “syrup” kutokana na kuchemsha ulanzi. Kama teknolojia hii itafanikiwa wakulima wa ulanzi watakuwa wamekombolewa kwani wataweza kuuza kwa faida bidhaa na mazao ya ulanzi.

 

 

Bwana Kayamba akiwa anagema ulanzi. 

 

 

 

 

 

 

 

 

Leave a Reply