Monday, July 20th, 2009

Vijana na maisha ya Kijijini

Evance Seth

Kijana Emanuel ni mzaliwa wa kijiji cha Iniho wilayani Makete. Toka kuhitimu kwake elimu ya msingi 1997 Emmanuel alikuwa akiishi kijijini Iniho kama vijana wengine wa kijijini akifanya shughuri za kujikimu ikiwemo kilimo mpaka mwaka 2003 aliposafiri kwenda Mufindi kutafuta kazi katika mashamba ya chai.

Bwana Emanuel alibahatika kupata kazi ya kuchuma chai katika mashamba hayo. Hata hivyo baada ya mwezi mmoja alishindwa kuendelea na hii na kazi tena. Kazi hii haikuweza kumpa kipato hata cha kukidhi mahitaji yake kwani kwa siku aliweza kuchuma chai kilo nne wakati kwa wastani mtu anachuma kilo mpaka mia moja. Kilo ya chai ilikuwa ikinunuliwa kwa shilingi mia mbili. “Niliamua kucha kazi hii kwa hiari yangu” alisema Emanuel alipokuwa akizungumza na mtandao huu. Alipoacha kazi Emanuel alienda kuomba kazi sehemu nyingine ambapo alipata kazi ya kufyaka vichaka na miti inayoota kando kando ya bara bara . Kazi hii ilikuwa inamuingizia kipato cha shilingi elfu moja na mia tano kwa siku na pia aliweza kuimudu hii kazi .

Baada ya miezi mitatu Emanuel tatu tangu ameanza kazi ya kuasafisha barabara alipata marafiki waliokuwa wamekuja likizo Mufindi wakaitokea Dar Es salaam. Marafiki hawa walikuwa ni waimbaji wa nyimbo za kizazi kipya maarufu kama bongo flava. Wana muziki hawa hakukawia kutambua kipaji cha uimbaji kilichofichika ndani ya Emanuel. Wakamtaka Emanuel ajiunge nao na waongozane kwenda Dar Es salaam.

Emanuel akasafiri na hao wasanii rafiki zake mpaka Dar Es Salaam ambako alifikia kwa mtu wa kijijini kwao ambaye ni mmiliki wa shule ya Nia Njema Mjini Dar Es Salaam. Mwenyeji wa Emanuel alimpa kazi ya kulisha Nguruwe na Kuku, kazi aliyotakiwa kufanya mchana mzima na kupumzika usiku. Kutoka na kuwa na kazi nyingi mchana hakupata nafasi ya kwenda kufanya mazoezi ya uimbaji na wenzake. Emanuel akatafuta namna atakavyoweza kutekeleza dhamira yake ya kuimba na siku moja awe miongoni mwa watu wanaong’ara katika anga za muziki na hatimaye kuwa na pesa za kuweza kujitegemea kama sio tajiri. Ilimlazimu Emanuel kutafuta muda zaidi ya mchana, akawa anatoroka usiku kwenda kufanya mazoezi na rafiki zake.

“Usiku mmoja nilipokuwa nimetoroka kwenda kwenye mazoezi ya uimbaji mwenyeji wangu akajua sipo, akafunga geti nyuma baada ya mimi kutoka” anaeleza Bwana Emanuel. Kurudi nyumbani asubuhi Emanuel anakumbana na geti lilofungwa.  Tajiri wa Emanuel alimwachisha kazi mara tu ya Emanuel Kufunguliwa geti kuingia ndani. Tajiri wake anampa masaa mawili awe amechukua kilicho chake na kuondoka kwenye viwanja vya mji wake. Mwenyeji wa Emanuel aliogopa kuwa huenda Emanuel akitoka usiku alikuwa akijihusisha na vitendo vya kijambazi.  Alimkabidhi shilingi elfu sabini ikiwa sehemu ya mishahara yake ya kufanya kazi, pesa ilikuwa inatosha kumrejesha mpaka nyumbani Makete.

Badala ya kwenda kijijini “Hata Hivyo sikwenda kituo cha mabasi Ubungo kunakopatikana usafiri wa kwenda Makete, niliamua kwenda kivukoni kuchukua usafiri wa Zanzibar kwasababu rafiki zangu walikuwa na safari ya kwenda kufanya onyesho Zanzibar”  . Emanuel alifika Zanzibar kwa kuchelewa rafiki zake walikuwa wameshamaliza tamasha na hawakuweza kumsubiri wakawa wamechukua boti ya kurudi bara.  Emanuel anafanya kosa la msingi badala ya kugeuza mara moja anakaa afurahie uzuri wa Zanzibar kidogo, anajikuta anamaliza pesa yote aliyokuwa amebakiwa nayo pale Rambo Motel alipofikia kisiwani Zanzibar.

Emanuel anashukuru kwani kabla ya kuishiwa mpaka nauli anaweza kurudi bara, anakofika mchana anaanza mara moja kuwatafuta rafiki zake maana muda huo alikuwa  hana kwa kula wa kulala, anapigwa na mshangao kuona jamaa zake hawapo Dar Es Salaama wanamtaarifu kuwa wapo Mwanza kushiriki kwenye onesho. Inamlazimu emanuel kutafuta kazi ili aweze kujikimu mpaka rafiki zake warudi. Baadaye anapata kazi ya muda kwa dada mmoja, anaye mpa chakula na mahali pa kuishi katika nyumba yake. Emanuel anaishi na huyu dada asiye na mume na baadaye wanaingia kwenye uhusiano na kushiriki ngono zembe. “Nimekaa naye miezi sita mpaka nilipopata habari za kufariki kwa mama yangu kijijini” anaeleza Emanuel kisha kilichomfany aachane na huyu dada. Baada ya kupokea taarifa za kufariki kwa mama yake Emanuel kwa kusaidiwa na mwenyeji wake wanatafuta nauli ya kumrudisha nyumbani, ambako yupo mpaka leo.

Alipoulizwa kama hana wasi wasi wa kuwa hana maambukizi ya UKIMWI kutokana na uhusiano wake Emanuel anasema kuwa amekuwa siku zote akihisi labda aliambukizwa na angependa kupima afya ili aweze kujitambua kama ameathirika au la. Alisema ameshindwa kupata huduma ya kupima kwani huduma ya hii inapatikana mbali mpaka hospitali ya Bulongwa ambayo bado mtu hana uhakika kama utapata huduma ukitembea umbali wote kuifuata.

Alipohojiwa uwezekano wa maambukizi Mganga wa PIUMA , Juma Nzige akiongea namtandao huu anasema vijana wengi wapo kwenye nafasi kubwa ya kuambukizwa maambukizi ya VVU kutokana na kutokuweza kuachana na ngono, au kuwa waaminifu au kutumia kinga. 

Akieleza upatikanaji wa huduma ya upimaji karibu na watu,  Bw. Nzige anasema shirika lake limejitahidi kusogeza huduma ya upimaji karibu na walengwa vijijini ili vijana kama Emanuel wanaoshindwa kuifuata huduma hiyo waipate. “Kama serikali ingeweka huduma za klinik inayotembea au kusaidia mashirika katika upimaji na utoaji wa dawa za ARV tungeweza kuwafikia watu wengi zaidi kuliko tunavyofanya sasa” anamalizia Juma Nzige.

Mwenyekiti wa kitongoji anapotokea Bw. Emanuel Bw. Mchaga aliuambia mtandao huu tatizo la vijana kuhamia mijini lina sura mbili. Sehemu moja ni ya kuwalaumu vijana wenyewe kwa kutokupenda shughuri za kilimo na kuishi kijijini wakifikiri wakienda mjini watapata kazi na maisha rahisi zaidi. Lakini pia anaitaka serikali na jamii kutoa msaada  zaidi wa kijamii na kiuchumi kwa vijana hasa baada ya kumaliza elimu zao ili waweze kuyakubali maisha ya kijijini.

Wilaya ya makete ni miongoni mwa wilaya zenye tatizo kubwa la uhamaji wa watu kutoka wilayani humo kwenda mijini kutafuta kazi pamoja na kuwa na maliasili nyingi kama za miti na aridhi nzuri yenye kustawisha mazao mengi na mvua zinazonyesha sehemu kubwa ya mwaka. 

Leave a Reply