Thursday, August 13th, 2009

Vijana wapewa stadi za maisha

Na Evance Seth

 

Wakati vijana wa kijiji cha iniho wakiendelea na semina nyingine kijijini kwao kama ilvyoripotiwa na mtandao huu, vijana wengine wa umri kati ya miaka kumi na nne hadi kumi na nane walikuwa wakipata elimu nyingine ya stadi za maisha kijijini Bulongwa.

 

Katika semina iliyofanyika ukumbi wa Dinduka kijijini Bulongwa iliratibiwa na wakufunzi Salum Sanga, afisa utamaduni wa wilaya ya Makete na Bw. Juma Sanga, afisa utamduni wa wilaya ya Makete iliwashirikisha vijana kutoka katika vijiji vyote vya tarafa za magoma na Bulongwa.

 

Vijana wawili kutoka katika kila kijiji walifanya jumla ya vijana sitini walioshiriki semina hiyo waliowawakilisha vijana wenzao wa kata nne za tarafa hizo mbili za Bulongwa na Magoma. 

 

Wakizungumza na mtandao huu kutoka katika ukumbi wa semina hiyo Vijana Mary Baghdad wa Iniho na Joseph Muvela wa kijiji cha Iyoka walisema “Hii semina ilikuwa na nia ya kuwapa vijana nyenzo za kukabiliana na mazingira hatarishi ya maambukizi ya UKIMWI”

 

“Tumejifunza namna ya kukabiliana na mihemko, mahusiano, kuwa wabunifu, ushirikeli na kujitambua,” walisema vijana hao. Wakizungumzia stadi ya kujitambua vijana hao walioungwa mkono na wenzao waliokuwa wamewazunguka wakati wa mahojiano na mwandishi walisema, stadi hii ni muhimu kwani inamfanya kijana ajijue anatoka wapi, yupo wapi , anafanya nini na anakwenda wapi.

 

Bw. Salum Sanga alisema wamefanya mafunzo na vijana walio chini ya miaka kumi na tisa kwasababu vijana wa umri chini ya miaka kumi na tisa wengi wao hawajapata nafasi ya kupata elimu ya stadi za maisha wakiwa nje ya mashule.

 

“Vijana wengi wa umri huu wametoka mashuleni hivi karibuni kwa hiyo kuna ulazima kuwapa elimu inayofanana na mazingira wanayoishi sasa, mazingira ya nje ya shule” alisema mkufunzi wa semina hiyo Bw. Sanga. Vijana hao wanategemewa kuwa mabalozi na kutoa elimu kwa vijana wenzao vijijini wanakotoka.

 

Vijana wakipata semina ya stadi za maisha

Vijana wakipata semina ya stadi za maisha

 

 

 

Leave a Reply