Friday, August 28th, 2009

Makete waanza kulima Pareto

Na Evance Seth.

 

Wananchi wilayani Makete wamekuwa na furaha tena baada ya zao la biashara la Pareto kuanza kununuliwa tena. Pareto ni zao pekee la biashara Wilayani Makete  lilitoweka baada ya kukosekana kwa soko.

 

Akizungumza na mwandishi wa habari hii mmoja wa wakulima wa zao hili Bwana Kensi alisema ”Nimeanza kulima zao hili mwaka 2007 baada ya kupata nguvu kutoka kwa  kampuni ya pareto walipokuja kijijini kwetu na kutuahidi soko la uhakika’’

 

Wanunuzi hao wa pareto wanatoa motisha na uhamasishaji kwa wakulima kulima kwa wingi zao hili kwa kuwapunguzia gharama za ukulima kwa kugawa mbegu bure kwa wanakijiji wakulima. Mbegu ambazo zimekuwa zikipatikana kwa watendaji wa vijiji bure hutolewa bila urasimu wote.

 

Bw. Kensi mmiliki wa shamba la ekari moja anavuna pareto yake kila wiki na hutumia siku tatu kukauka wakati wa kiangazi na wiki moja wakati wa msimu wa mvua. Aliendelea kusema bei ya kilo moja ya pareto ni sh. 900/= kwa hiyo kwa mwezi huwa anakusanya kilo zisizopungua arobaini.

 

“Nikishakausha pareto yangu huipeleka kwa Afisa kilimo ambapo hupimwa na kupewa pesa zangu keshi”. Alisema Bw. Kensi.

 

Kilimo cha pareto ni kilimo rahisi sana kwani hakihitaji mbolea na matunzo makubwa zaidi ya palizi inayofanywa mara mbili kwa mwaka. Na zao linalompatia mkulima pesa kila wiki.

 

Hata hivyo Bwana Kensi alisema kuwa matatizo madogo madogo ambayo huwa anayapata hasa wakati wa masika pareto hukuchukua muda mrefu kukauka kwani jua huwa linakuwa la shida, na mvua zikinyesha mfululizo husababisha pareto hiyo kuoza, na biashara yake kuwa sio nzuri.

 

‘’Pamoja na kuwa biashara sio nzuri malengo yangu ya baadaye ni kuongeza kulima mashamba mengine ya pareto, kwani pesa ninayopata inanikwamua kwenye matatizo madogo madogo ya kifamilia”alisema Bw. Kensi.

 

Ulimaji wa zao la preto ulistawi kuanzia miaka ya 1960 na kusimama miaka ya 1980 baada ya matumizi ya DDT kupigwa marufuku na hivyo pareto ambayo ilikuwa malighafi ya dawa hiyo kukosa soko.

 

Ingawa wakulima wa Makete hawajui pareto inatumika kwa ajili ya nini sasa, lakini wanashukuru kwasababu hivi sasa soko la Pareto limekuwa zuri kwani imeshaanza kupata soko kwenye soko la dunia.

Bwana Kensi akiwa anachuma pareto.

Bwana Kensi akiwa anachuma pareto.

One Response to “Makete waanza kulima Pareto”


  1. malila says:

    Kwa kweli ni hatua nzuri sana.Niliwahi kuona mashamba ya pareto zamani ktk maeneo ya Isapulano,ilikuwa raha. Nilipopita tena miaka ya juzi hapa sikuona kitu. Hongereni wote.

Leave a Reply