ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA
Na Evance Seth
Mwito wa serikali kwa wananchi wa elimu kwa wote umepokelewa kwa mikono miwili na wananchi Katika Wilaya ya Makete. Hayo yameonyeshwa na wananchi wa kijiji cha Ikovokovo waliojenga shule ya msingi iliyoanza tarehe 15 mwezi wa pili mwaka 2002.
Shule hiyo ilianza na wanafunzi hamsini na moja ikiwa na mwalimu Leonard Kyando aliyekuwa mwalimu pekee wa shule hiyo ambaye kwa sasa ni mwalimu mkuu msaidizi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Bw. Kyando alisema, Mwanzilishi wa wazo ni wananchi toka vitongoji vitatu navyo ni Ikovokovo, Kisiva na Masalala. Shule hii ilianza kwa mtaji wa nguvu za wananchi na kupata msaada uliotolewa na serikali kupitia mpango wa MEM utolewao kwa kila shule kujengewa jengo moja au mawili.
Kwa sasa shule inajumla ya walimu wanne na wanafunzi mia moja arobaini na moja kati yao wavulana 72 na wasichana 69.Pia shule hiyo inatoa elimu ya watu wazima mara mbili kwa wiki.
“Kwa mtu asiye penda kumpeleka mtoto shule tunampa elimu na kumshawishi mzazi au mlezi juu ya faida za elimu kwa mtoto kwa maisha ya baadaye kama akikaidi zaidi anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kama ataendelea kukataa hatampeleka mtoto shule” alisema Bw. Kyando.
Akizungumzia matatizo yanayoikabili shule hiyo, Bw. Kyando kwasasa tatizo la yatima bado ni kubwa kwani wanafunzi 40 ni yatima na 20 wanaishi katika mazingira magumu. “watoto hao hupewa msaada kidogo kama daftari na biki kutoka kwenye mashirika mbalimbali pamoja na walimu” aliongeza Bw. Kyando.
Changamoto zingine zinazoikabili shule hiyo ni pamoja na ukosefu wa maji, vyumba vya madarasa , nyumba za walimu ,vifaa vya michezo pamoja na zana za kufundishia. Walimu wa shule hiyo kwa pamoja walikiri kuwa taaluma kwa ujumla ni nzuri. “Malengo yetu kwa baadaye ni kuboresha taaluma na kuakikisha wanafunzi wote wanafaulu mtihani na kwenda sekondari.” Alisema Mwalimu Sanga

