Barabara Kukarabatiwa
Na Evance Seth
Wilaya ya Makete inaweza ikaepukana na adha ya tatizo sugu la bara bara kufikia mwakani. Hayo yamefahamika mwishoni mwa wiki iliyopita wakati naibu waziri wa miundo mbinu Mh. Hezekia Chibulinje akipokea taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo akiwa ziarani wilayani Makete.
Akisoma taarifa hiyo mkuu wa wilaya Bi. Hawa Ng’umbi amesema kuwa Halmashauri ya wilaya Makete imekuwa ikipokea fedha kutoka mfuko wa barabara ambazo zimekuwa hazitoshelezi mahitaji halisi ikilinganishwa na urefu wa barabara za Makete.
Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri wa miundo mbinu alikiri kuwepo kwa tatizo sugu la bara bara wilayani Makete kwa muda mrefu. Hata hivyo Mh. Chibulunje aliwapa matumaini viongozi wa wilaya waliofika kumpokea kwa kuwaambia kuwa serikali imesikia kilio cha wananchi wa Makete kwani barabara za wilaya ya Makete zitapata suruhisho la kudumu.
Mheshimiwa Chibulunje alitembelea maeneo kadhaa ya wilaya ya Makete kujionea ubovu wa Bara bara na utekelezaji wa miradi hiyo. Hata hivyo wananchi kadhaa waliozungumza na mtandao huu walionyesha wasi wasi wa matokeo ya tathmini atakayopata Mheshimiwa naibu waziri wa Miundo mbinu katika ziara yake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wachache waliohojiwa na mwandishi wetu walisema, kwa ujumla mtu hawezi kuona ubovu mkubwa wa bara bara wilayani makete kama atatembelea wilaya hii wakati wa kiangazi. Wananchi wengi walisema wilaya hii inayozungukwa na milima huwa haipitiki wakati wa masika kutokana na utelezi, matope na mashimo yanayosababishwa na mvua.
“angekuja wakati wa masika asikilizie mziki wake” alisema kijana Omega wa Mabehewani Makete akimaanisha mheshimiwa waziri aone ukubwa wa tatizo. “wakati wa masika huwezi kusafiri kwa gari wilayani Makete kwa zaidi ya Kilomita kumi bila kusukuma Gari lako” alimalizia kijana huyo.
Wapo wanachi wengine waliosema wanasubiri kuona matokeo ya utekelezaji wa mradi huu ndio watoe pongezi zao kwa naibu waziri na serikali.
