Vijana Makete Kusoma Ufundi
Na Evance Seth
Mkurugenzi mkuu wa VETA nchini Bwana. Zebadia Moshi akiwa ameongozana na baadhi ya wakurugenzi wa VETA nchini mwezi uliopita walikabidhiwa rasmi na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Makete mkataba wa kuanza kujengwa kwa chuo cha VETA wilayani Makete.
Akizungumza na Kitulo FM mwezi uliopita Bw. Moshi alisema kuwa mpango wa serikali ni kujenga vyuo 126 kwa awamu tatu katika wilaya zote hapa nchini, ambapo awamu ya kwanza vitajengwa vyuo thelathini, na Wilaya ya Makete ikiwa imepewa nafasi ya kwanza Kitaifa kuanza ujenzi wa chuo cha VETA.
Aidha ameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Makete kwa utekelezaji wa kutafuta hatimiliki pamoja na maandalizi ya miundo mbinu ya mahali kitakapojengwa chuo hicho.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Makete Bi. Hawa Humbi na mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mh. Ona Amosi Sikunala Nkwama amesema kuwa kujengwa kwa chuo hicho kutasaidia vijana wa Makete kupata elimu ya ufundi kwani mbao zinazouzwa nje ya wilaya zitaboreshwa kwa kutengeneza vifaa bora vitakavyouzwa ndani na nje ya Wilaya.
Jumla ya shilingi Bilioni tatu zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho kitakachokuwa kinatoa fani mbalimbali za ufundi.
