Latest News

September 28th, 2009

Barabara Kukarabatiwa

Na Evance Seth

Wilaya ya Makete inaweza ikaepukana na adha ya tatizo sugu la bara bara kufikia mwakani. Hayo yamefahamika mwishoni mwa wiki iliyopita wakati naibu waziri wa miundo mbinu Mh. Hezekia Chibulinje akipokea taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo akiwa ziarani wilayani Makete.

Akisoma taarifa hiyo mkuu wa wilaya Bi. Hawa Ng’umbi amesema kuwa Halmashauri ya wilaya Makete imekuwa ikipokea fedha kutoka mfuko wa barabara ambazo zimekuwa hazitoshelezi mahitaji halisi ikilinganishwa na urefu wa barabara za Makete.

 

Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri wa miundo mbinu alikiri kuwepo kwa tatizo sugu la bara bara wilayani Makete kwa muda mrefu. Hata hivyo Mh. Chibulunje aliwapa matumaini viongozi wa wilaya waliofika kumpokea kwa kuwaambia kuwa serikali imesikia kilio cha wananchi wa Makete kwani barabara za wilaya ya Makete zitapata suruhisho la kudumu.

 

Mheshimiwa Chibulunje alitembelea maeneo kadhaa ya wilaya ya Makete kujionea ubovu wa  Bara bara na utekelezaji wa miradi hiyo. Hata hivyo wananchi kadhaa waliozungumza na mtandao huu walionyesha wasi wasi wa matokeo ya tathmini atakayopata Mheshimiwa naibu waziri wa Miundo mbinu katika ziara yake.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wachache waliohojiwa na mwandishi wetu walisema, kwa ujumla mtu hawezi kuona ubovu mkubwa wa bara bara wilayani makete kama atatembelea wilaya hii wakati wa kiangazi. Wananchi wengi walisema wilaya hii inayozungukwa na milima huwa haipitiki wakati wa masika kutokana na utelezi, matope na mashimo yanayosababishwa na mvua.

 

“angekuja wakati wa masika asikilizie mziki wake” alisema kijana Omega wa Mabehewani Makete akimaanisha mheshimiwa waziri aone ukubwa wa tatizo. “wakati wa masika huwezi kusafiri kwa gari wilayani Makete kwa zaidi ya Kilomita kumi bila kusukuma Gari lako” alimalizia kijana huyo.

 

Wapo wanachi wengine waliosema wanasubiri kuona matokeo ya utekelezaji wa mradi huu ndio watoe pongezi zao kwa naibu waziri na serikali.

September 28th, 2009

Zoezi la kuandikisha wapiga kura

na Evance Seth

Wananchi wilayani Makete kwa muda wa siku tano mfululizo wameungana na watanzania wenzao wa mkoa wa Iringa kushiriki katika zoezi la kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura. Zoezi hili lilimhusu kila mwananchi mwenye umri wa kuanzia miaka kumi na nane na kuendelea  na mwenye akili timamu.

Akiongea na wananchi wa kata ya Iniho Mtendaji wa kata ya Iniho Bw. Christopher Fungo aliwaambia wananchi wa kata hiyo  kuwa umri wa miaka zaidi ya kumia na nane na akili timamu ndio sifa pekee za kumfanya mtu aandikishwe katika daftari la kudumu la wapiga kura

Akifafanua zaidi mtendaji huyo alisema “mtu ambaye hana kadi ya kupigia kura au endepo amepoteza  hataruhusiwi kupiga kura” hata Hivyo alizidi kusema watu wanaofikisha miaka hiyo wataandikishwa na kupewa kadi za kupigia kura na baadaye kuruhusiwa kushiriki katika zoezi la upigaji kura.

Kuhusu wapiga kura waliondikishwa lakini wamefariki mtendaji huoyo alisema kuwa kadi zao zinapswa kurudishwa kwa muandikishaji ili taarifa zao ziweze kufahamika.

Akiongea na mtandao huu mmoja wa wanachama wa PIUMA aliyejiandikisha katika zoezi hili Bw. Shem Kilemile alisema kupiga kura ni haki na niwajibu wa kila raia. “Nikiwa kama raia wa nchi hii nina haki ya kuchagua na kuchaguliwa, na ninaona ni wajibu wangu kutimiza haki hii” alisema Bwana Kilemile.

 

September 18th, 2009

WANACHAMA WA PIUMA WAALIKWA KUTEMBELEA KIKUNDI CHA CHAKUNIMU – NJOMBE.

 

 

Na Witness Ngumba.

 

Wanachama  watano  wa PIUMA wiki iliyopita walialikwa kwenda Njombe kuonana na kikundi cha CHAKUNIMU(Chama cha Kupambana na UKIMWI ,Nyumbanitu, Itulike, Mvelela, Ulembwe) ili kujifunza  na kubadilishana mawazo juu ya kuhudumia wagonjwa majumbani (HBC) na kujifunza kazi mbalimbali zinazofanya na kikundi hicho.

 

Wanachama hao wameenda kukaa siku kumi (10) na wanachama waliokwenda ni Markusi Chaula, Apolo Mbogela , Esterina Swalo, Anamere Pilla na Sabina Sanga.

 

Akizungumza na mwandishi wa habari hii mkuu wa msafala Bwana Markusi Chaula alisema kuwa matembezi hayo yalikuwa ya siku kumi na tumetembelea vijiji sita vyenye umbali wa kilomita 114,na wagonjwa tuliotembelea ni 84, vijiji vyote hivyo tulikuwa tunatembea kwa mguu.Vijiji vyote hivyo tuliongozwa na Lawrence Lilawola- Mwenyekiti wa CHAKUNIMU na Amoni Msigwa- Katibu wa CHAKUNIMU. Na jumla ya watu liokuwa tumeshiriki katika matembezi haya tulikuwa watu 30 tuliokuwa tumetoka sehemu mbalimbali.

 

Aliendelea kusema kuwa  kazi zinazofanywa na  kikundi cha CHAKUNIMU ni kuhamasisha jamii kwenda kupima Virusi vya Ukimwi kwa hiari, kuwatembelea wagonjwa majumbani katika vijiji vyote vilivyo ndani ya CHAKUNIMU.

 

Lakini kuna baadhi ya tofauti tulizoziona kati ya PIUMA na CHAKUNIMU, CHAKUNIMU ni kukundi cha watu mchanganyiko  waliopima Virusi vya Ukimwi na ambao hawajapima na wakati sisi PIUMA ni kikundi cha tuliopima na tunaishi na Virusi vya Ukimwi  na wao kituo cha kuchukulia dawa ni mbali sana sio sawa na sisi PIUMA. Pia wao hutembelea wagonjwa kila kijiji kilichopo ndani ya CHAKUNIMU wakati sisi PIUMa hatufanyi hivyo.

 

Baada ya kumaliza kutembelea vijiji sita tulikusanyika pamoja na kukaa kikao cha kutathimini kazi ilivyofanyika, wajumbe wa pande zote mbili walisema kuwa tumefanya kazi kubwa kwani watu wengi wamefurahi kuwatembelea  kwani wameelika sana juu yetu kwa kujieleza ni jinsi gani tunavyoishi na VVU na kutualika tena tuweze kuwatembelea kwa wakati mwingine.

 

Wanachama walioenda CHAKUNIMU - NJOMBE

Wanachama walioenda CHAKUNIMU - NJOMBE

 

 

 

 

September 10th, 2009

WANAPIUMA WAKUSANYIKA KUMKARIBISHA DR. ZIN ZIN.

 Na Witness ngumba.

 

Juzi tarehe 08/09/2009 ulifanyika Mkutano wa kumkaribisha Dr. zin zin na wanachama wa PIUMA pamoja na uongozi wao, mkutano huo ulifanyikia  kwenye jengo la PIUMA. Jumla ya wanachama waliohudhuria walikuwa 80 idadi hii ni kama nusu ya wanachama wote,  wanachama wengine walishindwa kufika kutokana na sababu mbalimbali walizotoa kwa katibu.

 

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Katibu Mkuu wa PIUMA  Bi. Anna Mwinuka “alisema kuwa ujio wa Dr. Zin Zin ni mzuri kwa sababu ameshaanza kufanya kazi na wanaPIUMA kama kuhudumia wagonjwa kwa utafiti wa ndani, hivyo wagonjwa wanaendelea kufarijika na kumiminika kwa kasi kwenda kituoni kupima afya zao kutokana na uwepo wake PIUMA. Amesema kuwa yupo  tayari kutufundisha wanaPIUMA kiingereza pamoja na kuanzika kwa kutumia Kompyuta. Na kwa nyuso za wanachama wengi walionyesha kufurahia ujio wake huyu daktari kwani siku hiyo baada ya kujitambulisha kwa jina la Dr. Zin Zin na kueleza malengo yake ya kuja PIUMA ni kufanya kazi na PIUMA hasa kwenye masuala ya afya, wanachama walifurahi na kuimba nyimbo kwa shangwe na vigelegele.

 

Kwa niaba ya wanaPIUMA wote tunapenda kutoa shukrani zetu kwa wale wote walioshiriki katika mchakato wa kumtafuta daktari huyu na hatimaye kumsafirisha na kufika PIUMA  kwani tumetambua kuwa tunapendwa na wafadhili  na mnautambua umuhimu wa afya zetu”alisema Katibu”.

 

WanaPIUMA wakisubiri mkutano kwenye jengo lao.

WanaPIUMA wakisubiri mkutano kwenye jengo lao.

Dr. zin Zin akizungumza na wanaPIUMA

Dr. zin Zin akizungumza na wanaPIUMA

 

WanaPIUMA wakiimba na kutawanyika.

WanaPIUMA wakiimba na kutawanyika.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

September 1st, 2009

ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA

Na Evance Seth

 

Mwito wa serikali kwa wananchi wa elimu kwa wote umepokelewa kwa mikono miwili na wananchi Katika Wilaya ya Makete. Hayo yameonyeshwa na wananchi wa kijiji cha Ikovokovo waliojenga shule ya msingi iliyoanza tarehe 15 mwezi wa pili mwaka 2002.

Shule hiyo ilianza na wanafunzi hamsini na moja ikiwa na mwalimu Leonard Kyando aliyekuwa mwalimu pekee wa shule hiyo ambaye kwa sasa ni mwalimu mkuu msaidizi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Bw. Kyando alisema, Mwanzilishi wa wazo ni wananchi toka vitongoji vitatu navyo ni Ikovokovo, Kisiva na Masalala. Shule hii ilianza kwa mtaji wa nguvu za wananchi na kupata msaada uliotolewa na serikali kupitia mpango wa MEM utolewao kwa kila shule kujengewa jengo moja au mawili.

Kwa sasa shule inajumla ya walimu wanne na  wanafunzi mia moja arobaini na moja kati yao wavulana 72 na wasichana 69.Pia shule hiyo inatoa elimu ya watu wazima mara mbili kwa wiki.

“Kwa mtu asiye penda kumpeleka mtoto shule tunampa  elimu na kumshawishi mzazi au mlezi juu ya faida za  elimu kwa mtoto kwa maisha ya baadaye kama akikaidi zaidi anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kama ataendelea kukataa hatampeleka mtoto shule” alisema Bw. Kyando.

Akizungumzia matatizo yanayoikabili shule hiyo, Bw. Kyando kwasasa tatizo la yatima bado ni kubwa kwani wanafunzi 40 ni yatima na 20 wanaishi katika mazingira magumu. “watoto hao hupewa msaada kidogo kama daftari na biki kutoka kwenye mashirika mbalimbali pamoja na walimu” aliongeza Bw. Kyando.

Changamoto  zingine zinazoikabili shule hiyo ni pamoja na ukosefu wa  maji, vyumba vya madarasa , nyumba za walimu ,vifaa vya michezo pamoja na zana za kufundishia.  Walimu wa shule hiyo kwa pamoja walikiri kuwa taaluma kwa ujumla ni nzuri. “Malengo yetu kwa baadaye ni kuboresha taaluma na kuakikisha wanafunzi wote wanafaulu mtihani na kwenda sekondari.” Alisema Mwalimu Sanga 

Wanafunzi wa shule ya Msingi Ikovokovo

Wanafunzi wa shule ya Msingi Ikovokovo

August 28th, 2009

PIUMA BUIDING TO DATE

slowly we can!

upper floor

upper floor

 

windows and door flem
windows and door flem

August 28th, 2009

Makete waanza kulima Pareto

Na Evance Seth.

 

Wananchi wilayani Makete wamekuwa na furaha tena baada ya zao la biashara la Pareto kuanza kununuliwa tena. Pareto ni zao pekee la biashara Wilayani Makete  lilitoweka baada ya kukosekana kwa soko.

 

Akizungumza na mwandishi wa habari hii mmoja wa wakulima wa zao hili Bwana Kensi alisema ”Nimeanza kulima zao hili mwaka 2007 baada ya kupata nguvu kutoka kwa  kampuni ya pareto walipokuja kijijini kwetu na kutuahidi soko la uhakika’’

 

Wanunuzi hao wa pareto wanatoa motisha na uhamasishaji kwa wakulima kulima kwa wingi zao hili kwa kuwapunguzia gharama za ukulima kwa kugawa mbegu bure kwa wanakijiji wakulima. Mbegu ambazo zimekuwa zikipatikana kwa watendaji wa vijiji bure hutolewa bila urasimu wote.

 

Bw. Kensi mmiliki wa shamba la ekari moja anavuna pareto yake kila wiki na hutumia siku tatu kukauka wakati wa kiangazi na wiki moja wakati wa msimu wa mvua. Aliendelea kusema bei ya kilo moja ya pareto ni sh. 900/= kwa hiyo kwa mwezi huwa anakusanya kilo zisizopungua arobaini.

 

“Nikishakausha pareto yangu huipeleka kwa Afisa kilimo ambapo hupimwa na kupewa pesa zangu keshi”. Alisema Bw. Kensi.

 

Kilimo cha pareto ni kilimo rahisi sana kwani hakihitaji mbolea na matunzo makubwa zaidi ya palizi inayofanywa mara mbili kwa mwaka. Na zao linalompatia mkulima pesa kila wiki.

 

Hata hivyo Bwana Kensi alisema kuwa matatizo madogo madogo ambayo huwa anayapata hasa wakati wa masika pareto hukuchukua muda mrefu kukauka kwani jua huwa linakuwa la shida, na mvua zikinyesha mfululizo husababisha pareto hiyo kuoza, na biashara yake kuwa sio nzuri.

 

‘’Pamoja na kuwa biashara sio nzuri malengo yangu ya baadaye ni kuongeza kulima mashamba mengine ya pareto, kwani pesa ninayopata inanikwamua kwenye matatizo madogo madogo ya kifamilia”alisema Bw. Kensi.

 

Ulimaji wa zao la preto ulistawi kuanzia miaka ya 1960 na kusimama miaka ya 1980 baada ya matumizi ya DDT kupigwa marufuku na hivyo pareto ambayo ilikuwa malighafi ya dawa hiyo kukosa soko.

 

Ingawa wakulima wa Makete hawajui pareto inatumika kwa ajili ya nini sasa, lakini wanashukuru kwasababu hivi sasa soko la Pareto limekuwa zuri kwani imeshaanza kupata soko kwenye soko la dunia.

Bwana Kensi akiwa anachuma pareto.

Bwana Kensi akiwa anachuma pareto.

August 28th, 2009

Upimaji wa Aridhi

Na Evance Seth

 

Wilaya ya Makete imeungana na wilaya zingine za Tanzania katika zoezi la kitaifa la upimaji wa Aridhi na viwanja. Zoezi hili linaratibiwa na kuendeshwa na Mpango wa Kurasimisha Rasimali na Biashara za wanyonge Tanzania (MKURABITA).

 

Akizungumza na mtandao huu mwenyekiti wa kijiji cha Iniho Bw. Ferance Sanga alisema zoezi hili limeanza katika wilaya ya Makete mwezi April. Hata hivyo Bw. Sanga alisema mvua zilizokuwa zikinyesha wakati wa masika zilipunguza kasi ya upimaji wa viwanja na mashamba.

 

Alipohojiwa na Mtandao huu kama anaona faida zozote za zoezi hilo Bi. Roda Muhando alisema, upimaji unawasaidia watu kuwa na hati ya umiliki wa mali zao. “kukatia hati miliki hiyo ni faida kwako kwani hakuna mtu atakaye kupokonya  shamba lako kwani utakuwa umekatia hati miliki na litatambuliwa ni la kwako” aliongeza Bi. Muhando.

 

Bi. Roda aliwaasa wanawake kujitokeza kwa wingi kupewa hati za kumiliki mashamba na Viwanja  kwani inawapa nguvu wanawake. “Nikiwa mwanamke nashukuru Serikali kwa kuanzisha huu mpango kwani sasa sitanyanyaswa kutokana na jinsia yangu kwenye umiliki wa aridhi” aliendelea kusema Mama Muhando.

 

Pamoja na zoezi la upimaji shirika pia litasaidiana na wanachi kujenga ofisi kwa ajili ya matumizi ya maofisa wa kijiji, baraza la aridhi na maofisa wa aridhi. Katika ujenzi huo wananchi watachangia nguvu, uwanja na mawe kwa ajili ya ujenzi na gharama zingine zote zitagharamiwa na MKURABITA.

haya ni baadhi ya mashamba yaliyopimwa.
Sehemu ya Mashamba yaliyopimwa Kijijini Bulongwa

Picha na Witness

August 13th, 2009

Vijana wapewa stadi za maisha

Na Evance Seth

 

Wakati vijana wa kijiji cha iniho wakiendelea na semina nyingine kijijini kwao kama ilvyoripotiwa na mtandao huu, vijana wengine wa umri kati ya miaka kumi na nne hadi kumi na nane walikuwa wakipata elimu nyingine ya stadi za maisha kijijini Bulongwa.

 

Katika semina iliyofanyika ukumbi wa Dinduka kijijini Bulongwa iliratibiwa na wakufunzi Salum Sanga, afisa utamaduni wa wilaya ya Makete na Bw. Juma Sanga, afisa utamduni wa wilaya ya Makete iliwashirikisha vijana kutoka katika vijiji vyote vya tarafa za magoma na Bulongwa.

 

Vijana wawili kutoka katika kila kijiji walifanya jumla ya vijana sitini walioshiriki semina hiyo waliowawakilisha vijana wenzao wa kata nne za tarafa hizo mbili za Bulongwa na Magoma. 

 

Wakizungumza na mtandao huu kutoka katika ukumbi wa semina hiyo Vijana Mary Baghdad wa Iniho na Joseph Muvela wa kijiji cha Iyoka walisema “Hii semina ilikuwa na nia ya kuwapa vijana nyenzo za kukabiliana na mazingira hatarishi ya maambukizi ya UKIMWI”

 

“Tumejifunza namna ya kukabiliana na mihemko, mahusiano, kuwa wabunifu, ushirikeli na kujitambua,” walisema vijana hao. Wakizungumzia stadi ya kujitambua vijana hao walioungwa mkono na wenzao waliokuwa wamewazunguka wakati wa mahojiano na mwandishi walisema, stadi hii ni muhimu kwani inamfanya kijana ajijue anatoka wapi, yupo wapi , anafanya nini na anakwenda wapi.

 

Bw. Salum Sanga alisema wamefanya mafunzo na vijana walio chini ya miaka kumi na tisa kwasababu vijana wa umri chini ya miaka kumi na tisa wengi wao hawajapata nafasi ya kupata elimu ya stadi za maisha wakiwa nje ya mashule.

 

“Vijana wengi wa umri huu wametoka mashuleni hivi karibuni kwa hiyo kuna ulazima kuwapa elimu inayofanana na mazingira wanayoishi sasa, mazingira ya nje ya shule” alisema mkufunzi wa semina hiyo Bw. Sanga. Vijana hao wanategemewa kuwa mabalozi na kutoa elimu kwa vijana wenzao vijijini wanakotoka.

 

Vijana wakipata semina ya stadi za maisha

Vijana wakipata semina ya stadi za maisha

 

 

 

August 13th, 2009

Vijana na UKIMWI

Na Evance Seth

 

Wiki hii vijana wapatao ishirini wa kijiji cha Iniho wamefaidika na elimu juu ya ugonjwa wa UKIMWI. Elimu iliyotolewa katika semina iliyowashirikisha vijana kuanzia miaka kumi na tano.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii mkufunzi wa semina hiyo Bw. Maonyesho Ngohani alisema semina hiyo ililenga kuwajengea uwezo vijana hao  wa kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoambatana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

“UKIMWI huleta madhara kwa mtu binafsi, familia yake na jamii kwa ujumla kwa hivyo ni muhimu kuwapa vijana nyenzo  na stadi za maisha kuweza kukabiliana na madhara hayo” alisema Bw. Ngohani. Mada nyingine iliyotolewa ilikuwa ni pamoja na namna ya kuwatunza walioathirika na VVU pamoja na kuondoa Unyanyapaa.

Akizungumzia sehemu za stadi za maisha za kuwakinga na VVU vijana Bw. Ngohani alieleza kuwa vijana hawana budi kujishirikisha na michezo, pia kushiriki katika shughuri za kimaendeleo zitakazo wainulia vipato vyao. Alisema ajira kwa vijana, vifaa na viwanja ya michezo ni changamoto mojawapo inayowakabili vijana katika kushiriki kikamilifu kwenye mapambano ya VVU.

“Tunawashauri vijana kuendelea kushikiria na kufuata ABC za kuepuka maambukizi ya VVU” alisema Mkufunzi huyo. Akizitaja ABC hizo bwana Ngohani alisema vijana lazima wajiepushe na Ngono, wawe waaminifu kwa wapezi wao na kutumia kondomu kila wanapofanya tendo la ngono. “Kila mtu ana mchango katika mapambano dhidi ya UKIMWI” alimalizia Bw. Ngohani.

 

“Vijana tunahitaji kujitambua na kujua umuhimu wetu katika mapambano dhidi ya UKIMWI” alisema Eva Lufingo mmoja wa washiriki wa semina hiyo. Akifafanua zaidi kijana huyo alisema vijana wana nyenzo na uwezo wa kutokomeza UKIMWI na kuasa jamii kuwa iwape nyenzo na nafasi ya kushiriki kwenye mapambano ya dhidi ya UKIMWI